Mshambuliaji mpya wa Yanga, Yohana Nkomola, juzi Jumatano alianza rasmi mazoezi na kikosi hicho katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo amekabidhiwa jezi namba 31.
Nkomola amesajiliwa na kikosi cha Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo, ameungana na timu hiyo kwa mara ya kwanza akitokea kwenye michuano ya Chalenji nchini Kenya akiwa na kikosi cha Kilimanjaro Stars.
Straika huyo amesema kuwa amefurahi kuungana na kikosi hicho na kuanza mazoezi mara baada ya kutoka kwenye michuano ya Chalenji nchini Kenya baada ya kurejea nchini Jumanne ya wiki hii.
“Sina tatizo na namba 31 lakini hata wakinipa jezi nyingine nitavaa, sichagui kwa sababu jezi haichezi, lakini pia nimepewa jezi hii baada ya nyingine zote kuwa na watu,” alisema Nkomola.
Kwa mara ya kwanza mshambuliaji huyo ataonekana kwenye kikosi cha Yanga, kesho ambapo timu hiyo itakuwa ikivaana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam