Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC kesho watacheza mchezo wa kirafiki na African Lyon ya Daraja la Kwanza Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
Mchezo huo ni maalum kuendelea kukiweka kikosi sawa kabla ya kurejea kwa mechi za Ligi Kuu, zilizopisha michuano ya CECAFA Challenge inayoelekea ukingoni nchini Kenya.
Na mchezo huo unakuja wiki moja baada ya Simba kushinda 3-1 dhidi ya timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC katika mchezo mwingine wa kirafiki huko huko Chamazi.
Siku hiyo, KMC inayofundishwa na kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Freddy Felix Minziro, ilitangulia kupata bao lililofungwa na Reyman Mgungila dakika ya saa kwa shuti la mpira wa adhabu nje kidogo ya 18, kabla ya Simba kutokea nyuma na kushinda 3-1.
Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco mawili, moja kwa penalti dakika ya 27, baada ya Mohamed Ibrahim 'Mo' kuangushwa ndani ya penati boksi na lingine dakika ya 86, ambalo lilikuwa la tatu baada ya winga Mzambia, Jonas Sakuwaha aliye kwenye majaribio kufunga la pili dakika ya 39.
Katika mchezo wa kesho Simba inatarajiwa kuongezewa nguvu na wachezaji wake waliokuwa kwenye kikosi cha Tanzania, Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya CECAFA Challenge.