WAKATI ripoti ya Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ikimworodhesha mshambuliji wa Mbao FC, Habibu Kyombo ili asajiliwe katika dirisha hili dogo la usajili, msaidizi wake, Masoud Djuma, amezuia straika huyo kupewa kandarasi.
Simba walianza kumfukuzia Kyombo kipindi cha usajili wa dirisha kubwa la Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini walishindwa kukamilisha hilo kutokana na kutoelewana baina yao na Mbao FC, alikokuwa na mkataba wa mwaka mmoja na hivyo kupanga jambo hilo kulitekeleza kwenye dirisha dogo.
Katika usajili unaofungwa leo saa sita usiku, jina la Kyombo liliwekwa tena kwenye orodha na kocha Omog, lakini rasmi Jumatatu iliyopita Simba walimpa taarifa mchezaji huyo kuwa hawawezi kumsajili kwa madai kocha msaidizi ameliondoa jina lake.
Akizungumza na MASENGWA BLOG, Kyombo alisema kuwa, alikuwa kiwasiliana na viongozi wa Simba waliokuwapo ndani ya Kamati ya Usajili tangu dirisha dogo lifunguliwe na kuzungumza juu ya kumpa mkataba wa miaka miwili.
“Tulishazungumza juu ya kunipa mkataba ili nikacheze, tena wakinisisitiza nisisaini sehemu nyingine, lakini mwanzoni mwa wiki hii ndipo nilipopewa taarifa kuwa hawataweza kufanya hivyo.
“Kiongozi aliyenipa taarifa hizo hakuweza kunieleza nini sababu, ukizingatia tulishazungumza masuala yote ya kimkataba, lakini watu wengine waliokuwapo ndani ya Simba, ndio wameniambia kocha msaidizi ameliondoa jina langu akihitaji kuniangalia zaidi kwenye mechi za ligi zilizobaki ili aone nitawafaa au la, hivyo nitaendelea kucheza katika timu yangu ya Mbao FC,” alisema.
Bingwa ilimtafuta Djuma kuzungumzia suala hilo, ambapo muda wote simu yake haikuwa ikipokewa na wakati mwingine kutopatikana.