Wakati Simba ikitaka kuyatumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi ili kupooza hasira za kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA, Uongozi wa Yanga umetangaza vita kwa watani wao kwa kutangaza mkakati wa kunyakua kombe hilo.
Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema timu hiyo itapeleka kikosi kamili Visiwani Zanzibar ambako mashindano hayo yatafanyika lengo likiwa ni kuchukua ubingwa.
"Baada ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Mbao, timu itaondoka Mwanza Jumatatu asubuhi kwenda Zanzibar. Tutapeleka kikosi kizima Zanzibar ili kuwapa burudani wapenzi wa soka na kuhakikisha tunatwaa ubingwa kwa sababu utamaduni wa Yanga ni kuchukua makombe.
Mkakati wetu kwenye mashindano hayo ni kutwaa ubingwa. Tunaamini timu zilizopo kwenye mashindano hayo ni nzuri lakini tutadhihirisha kwamba sisi ni mabingwa," alisema Ten.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umeiomba Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kushughulikia marekebisho ya miundombinu ya Majitaka ambayo imekuwa kero na kikwazo katika ukarabati wa Uwanja wa Kaunda
"Katika kipindi cha nyuma kuna mtaro ambao walikuwa wameuweka hapo nadhani mkandarasi alikuwa anautengeneza ukaishia njiani. Yale maji ambayo yanadondoka pale hayaendi katika mtiririko unaotakiwa, matokeo yale maji taka yanayotoka Kariakoo, yanakuja yanazunguka kuna uwazi na kujaa kwenye uwanja na kusababisha paonekane kama bwawa la majitaka.
"Tumejaribu kuwapelekea halmashauri lakini hatupewi ushirikiano. Sasa tumejaribu kufikisha hili ili wahusika walishughulikie na kama ikishindikana tutalifikisha kwenye vyombo vya kisheria," alisema Mkwasa