KOCHA WA SIMBA AZUA BALAA HUKO MISRI, ASEMA TUNAANZA UPYA



KOCHA mkuu wa Simba, Zoran Maki amewaambia wachezaji kuwa atakayefanya vizuri ndiye atakayepata nafasi ya kucheza bila kujali ukubwa wa majina.

Kauli hiyo ni kama amewatangazia kwamba kikosi chake kinaanza upyaa chini yake ili kurejesha ubabe wao Ligi Kuu Bara.

Hayo yamesemwa na kocha msaidizi wa timu hiyo ambayo imepiga kambi yake nchini Misri, Seleman Matola akielezea namna ambavyo wanaendelea na maandalizi.

Matola alisema Zoran amekuwa kama kocha mzoefu na mwenyeji ndani ya kikosi hicho kwani hata falsafa ya ufundishaji inaendana na mwongozo wa klabu. “Kocha amewaambia (wachezaji) hataangalia nani alikuwepo msimu uliopita na alifanya nini. Mchezaji atakayefanya vizuri ndiye atakayepata nafasi ya kucheza hivyo kila mmoja anajituma,” alisema Matola.

“Ukiangalia ushindani ndani ya timu ni mkubwa kila namba ina mtu na mtu, hivyo hapo ni kila mmoja kujituma na kuongeza juhudi zaidi maana wale ambao tuliona msimu uliopita hawakupata nafasi kubwa kucheza wanajituma zaidi na wale wengine hivyo hivyo.”

Kuhusu maendeleo ya kambi Matola alisema: “Ukiangalia tulivyoanza na tunavyoendelea kuna mapokeo makubwa kwa wachezaji, tunaamini ushindani utaongezeka.”ADVERTISEMENT


“Pia Kamati ya Usajili imetupatia wachezaji kulingana na upungufu tuliokuwanao. Imesajili wachezaji wazuri, wameletwa ambao kiukweli watakwenda kukidhi haja ya wana Simba,” alisema Matola na kwamba leo watacheza mechi ya tatu ya kirafiki dhidi ya Haras El Hodoud

OUATTARA APANIA

Beki mpya wa Simba, Mohamed Quattara ambaye pia yupo kambini ameonekana kuwa kamili kuhakikisha msimu utakapoanza anatoa huduma sahihi kikosini, huku akitamba kuwa Simba ijayo itakuwa moto.

Amesema kabla ya kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Al Hilal ya Sudan, alikuwa anaijua Simba ilivyo na mashabiki wenye vaibu kubwa kuwafanya wachezaji kupata morali ya kufanya kazi vizuri.

Al Hilal iliwahi kualikwa kucheza michuano ya Simba Super Cup 2021 na ndizo nyakati zilizompa picha kamili ilivyo Msimbazi beki huyo.

“Najua ni klabu kubwa iliyo na wachezaji wenye viwango vya juu, hivyo nimejiandaa kukabiliana na kila changamoto ya ushindani kuhakikisha naisaidia timu kutimiza malengo yake,” alisema.

“Najua ina mabeki wazuri ingawa niliyekuwa namfahamu ni Pascal Wawa, pia yupo Inonga (Henoc) ambaye nimemkuta, hivyo naamini tutafanya kazi nzuri kwa pamoja.”

Quattara ambaye nje ya kucheza beki ya kati anaimudu nafasi ya kiungo mkabaji, alisema inafurahisha kuona ndani ya Simba katokea staa Ousmane Sakho aliyechukua tuzo ya bao bora la Afrika.

“Ni namna gani Simba ina wachezaji wenye uwezo mkubwa unaonifanya nipambane kuna ushindani wa hali ya juu. Nafurahia kuwa sehemu ya kikosi cha Simba,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.