Mwenyekiti wa Kamtai ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ametoa zawadi ya gari kwa mchezaji wa Simba, Said Hamis Ndemla.
Hans Poppe ametangza kumpa Ndemla gari baada ya kuonyesha kiwango kizuri cha kuvutia katika mechi dhidi ya Singida United.
Simba imeshinda kwa mabao 4-0 katika mechi hiyo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini. Ndemla alitengeneza mabao mawili moja akifunga Emmanuel Okwi na jingine Asante Kwasi.
Hans Poppe amesema mechi ya leo imekuwa ni fainali ya uamuzi wake lakini amekuwa akimfuatilia Ndemla.
“Nilikuwa nikimfuatilia kama ambavyo nimekuwa nikisema nahitaji mchezaji mwenye nidhamu na ambaye hawezi kubadilika. Utaona Ndemla amekuwa benchi lakini akiingia uwanjani anaonyesha mchango wake,” alisema.
“Tena pamoja na kukaa benchi, hakuwahi kuonyesha utovu wa nidhamu. Badala yake kila akipata nafasi amekuwa akijituma na kuisaidia timu.”
Hii ni mara ya pili Hans Poppe anatoa gari kwa mchezaji wa Simba. Alianza na Hussein Zimbwe aliyempa gari aina ya Toyota Raum. Lakini akaonyesha gari aina ya Toyota Lactic na kusema atapewa mchezaji atakayefanya vizuri.
Kuhusiana na aina, amesema: “Aina utaijua baadaye ila gari haiko mbali. Hivyo tutaangalia siku yenye nafasi atakabidhiwa.”