KUELEKEA mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmerie kutoka Djibouti, Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre, amesema anataka kuimarisha eneo moja kwenye kikosi chake ili kuweza kuwakabili vyema wapinzani wao.
Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa itaumana na wageni hao Februari 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari Tandika, jana, Lechantre, alisema kuwa anataka kuona safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo keshokutwa itakutana na Ruvu Shooting inaimarika zaidi kuliko ilivyo sasa.
Lechantre alisema kuwa amefanikiwa kuangalia mikanda ya video ya wapinzani wao na kuona ni timu inayocheza kwa nidhamu ya mpira kwenye idara yao ya ulinzi.
“Katika mazoezi kwa sasa naweka mkazo kwenye safu yangu ya ushambuliaji, nataka tuwe na mbinu nyingi za kufunga hasa tunapokutana na timu yenye safu imara ya ulinzi, nalifanyia kazi hili,” alisema Lechantre.
Aliongeza kuwa anaridhishwa na namna wachezaji wake wanavyojituma kwenye mazoezi ya timu na anaamini watafanya vizuri kwenye michuano hiyo ya kimataifa ya CAF.
“Nafurahia hali ya kujituma kwa wachezaji, unaweza kuona namna wanavyofurahia mazoezi kwa kuyafanya kwa usahihi, nina wachezaji wazuri na hii itarahisisha kazi yangu,” aliongeza kocha huyo.
Okwi amtesa Mseja Katika mazoezi ya juzi, Emmanuel Okwi, alikuwa burudani kwa mashabiki kutokana na jinsi alivyokuwa akicheza kufuatia Lechantre kuigawa timu katika vikosi viwili, cha kwanza kikiwa na washambuliaji, John Bocco na Okwi, Shiza Kichuya huku kikosi cha pili golini akisimama Emmanuel Mseja.
Kivutio kikubwa kilikuwa kwa Okwi ambaye alikuwa na kasi kuelekea golini kila alipokuwa akipata mpira ambapo mara kwa mara alikuwa ‘akimtesa’ Mseja kwa mashuti au hata kumpiga chenga.